ADHABU KWA MAAJUZA KWA MISINGI YA USHIRIKINA NA UCHAWI KATIKA JAMII YA ABAGUSII NA JACKLINE NJERI MURIMI, CHUO KIKUU CHA TOM MBOYA ABSTRACT Licha ya teknolojia kutoa nafasi kwa kila mmoja kuwa sehemu ya mabadiliko yanayoendelea, inasikitisha kuwa baadhi ya watu barani Afrika wameamua kukwamilia katika ukale na tamaduni hafifu zilizopitwa na wakati. Uchawi ni mojawapo ya shughuli inayotekelezwa na wanaume na wanawake katika desturi za jamii nyingi za kiafrika ikiwemo ile ya Abagusii nchini Kenya. Hata hivyo hivi karibuni kumetokea hali ambapo adhabu kali imetolewa kwa wachawi maajuza katika jamii ya Abagusii jambo ambalo lilipelekea kuzuka kwa ghadhabu kali kutoka kwa wananchi na mashirika ya umma yakikemea ubaguzi huu. Mathalan, mifano halisi ya ukale huo ni mtindo wa baadhi ya vijana kuwachoma na kuwashambulia maajuza kwa kisingizio cha kuendeleza uchawi na ushirikina. Hivyo utafiti huu ulinuia kuchanganua adhabu ya uchawi na jinsia ya kike katika Jamii ya Abagusii suala ambalo limeonekana kuwakera wananchi na serikali kwa ujumla. Ubaguzi wa jinsia ya kike wakati wa kuwaadhibu wachawi umeonekana kuzua utegano, mafarakano, chuki na hata kuyaweka maisha ya wanawake hawa hatarini. Hivyo basi utafiti huu uliangazia utekelezaji wa adhabu kwa wachawi maajuza katika jamii ya Abagusii aidha na kutathmini madhara yake. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya ufeministi na uhalisia ajabu ambapo mihimili ya nadharia hizi ilitusaidia kufikia lengo kuu la utafiti huu. Katika kukusanya data mtafiti alitumia utafiti wa maktaba na ule wa mtandaoni pale ambapo data ya kimsingi ilipatikana kutokana na tasnifu zilizoandikwa kuhusu jamii ya Abagusii. Vilevile, utafiti wa nyanjani ulitumika pamoja na mbinu ya kimaelezo katika kuchambua data na kuiwasilisha kwa lugha ya kinathari kuambatana na malengo ya utafiti. Maarifa yaliyo katika utafiti huu yatakuwa mchango katika maarifa yaliyopo kuhusu masuala ya jinsia katika jamii.Zaidi ya hayo,utafiti huu utasaidia katika kuibua mapendekezo ambayo yatasaidia watengenezaji sera wanaojihusisha na suala la ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wanawake. KEY WORDS: Adhabu, Uchawi, Maajuza IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 10 1.0 Utangulizi Utafiti huu unachunguza adhabu inayotolewa kwa maajuza kwa misingi ya ushirikina na uchawi katika jamii ya Abagusii.Imani kuhusu uchawi na wachawi umekita mizizi nchini Kenya haswa katika kaunti ya kisii na bara la Afrika kwa ujumla na imani hii inaendelea kuwepo. Inaamika kuwa, mambo mengi yanayotendeka haswa ajali za barabarani, vifo vya watoto wachanga na watu wengine na magonjwa chanzo chake ni uchawi. Ni suala la kusikitisha mno wakati huu dunia inashuhudia mabadiliko mengi ya kiteknolojia ambapo ni vigumu kudhani kizazi cha sasa kinaweza kushabikia na kuendeleza baadhi ya tamaduni ambazo zimepitwa na wakati. Kwa mujibu wa Kamau Wanderi (2021), mabadiliko yanayoendelea yanapaswa kukifungua macho kizazi hiki kufahamu kuwa hakipaswi kuachwa nyuma dunia inapoendelea kubadilika. Inasikitisha kuwa baadhi ya vijana barani Afrika wameamua kukwamilia katika ukale na tamaduni dhaifu ambazo hazina maana yoyote katika maisha ya kisasa. Mifano halisi ya ‘ukale’ huo ni mtindo wa baadhi ya vijana kuwachoma na kuwashambulia wazee kwa kisingizio cha kuendeleza uchawi na ushirikina. Nchini Kenya katika kaunti ya Kisii maajuza ndio wanaosingiziwa kuwa wachawi zaidi na sio wanaume. Maajuza hawa wamekuwa wakidhulumiwa na hata kuuwawa katika jamii hii. Huku visa vya wazee kwa tuhuma za uchawi vikiendelea kukithiri haswa katika kaunti ya kisii, imebainika kuwa wanaotekeleza vitendo hivyo wanavunja sheria yenye adhabu kali. Maswali yanayoibuka ni: Ni vigezo vipi wanavyotumia wale wanaowashambulia wazee ili kubaini wanaendeleza maovu hayo? Kuna nguvu ama uwezo maalum walio nao? Bila shaka kitendo hiki ni cha unyama na kulingana na sheria iliyopo sasa yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kumsingizia mwenzake kuwa mchawi atatozwa faini ya laki tano au asukumwe gerezani kwa miaka mitano. Hii ni kulingana na sheria za kuhusu uchawi sura ya 67 ambayo pia inaharamisha vitendo vya uchawi au ushirikina. Kwa kauli hii, simaanishi visa na vitendo vya uchawi na ushirikina havipo. La hasha! Vipo kwa wingi. Hata hivyo, taratibu za kisheria zinapaswa kufuatwa kuchunguza na kubaini ikiwa ni kweli washukiwa wanaendesha maovu hayo au la. IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 11 Matokeoya Utafiti YafuatayonimawasilishoyamatokeoyamajibuyahojajikuhusumtazamowajamiiyaAbagusiikuhusua dhabuinayotolewakwamaajuzakwatuhumazauchawinaushirikina Jedwali1: AdhabukwawachawininjiamwafakayakupunguzavitendovyauchawikatikajamiiyaAbagusii Kauli 5 % 4 % 3 % 2 % 1 % Adhabu kwa wachawi ni njia mwafaka ya kupunguza vitendo vya uchawi katika jamii ya Abagusii 8 9 2 2.2 1 1.1 70 78.7 8 9.0 5-Nakubali kabisa, 4-Nakubali kiasi. 3-Nakubali, 2-Sikubali 1-Sina uhakika Chanzo: Ukokotozi wa mtafiti Kutokana na uchanganuzi wa data, watafitiwa 70 (78.7%) hawakukubaliana na maoni kuwa adhabu kwa wachawi ni njia mwafaka ya kupunguza vitendo vya kichawi katika jamii ya Abagusii huku watafitiwa 8(9.0%) wakikosa uhakika.Vilevile, idadi ndogo ya wahojiwa 8(9%) walikubali kabisa kuhusu madai hayo , wahojiwa 2(2.2%) wakikubali kiasi huku mhojiwa 1(1.1%) akikubali tu. Hivyo basi, kutokana na matokeo ya utafiti ni ukweli kwamba adhabu ya uchawi haipunguzi vitendo vya kichawi katika jamii ya Abagusii mbali ni vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake wazee.Tabia hii ya kishenzi na ukatili kawaida huidhinishwa na baadhi ya wanajamii ambapo vitendo hivi vimekithiri.Kutokana na data tuliyokusanya, wanafamilia wa maajuza hawa hushirikiana kuanzisha vurugu dhidi ya wanawake na hata mauaji ya maajuza hawa.Vilevile, adhabu hii husababisha familia za maajuza hawa kutengwa na jamii na uharibifu wa mali pale ambapo adhabu inahusisha kuchomwa kwa maajuza hawa pamoja na mali yao. Utekelezaji wa Adhabu kwa Wachawi Maajuza katika Jamii ya Abagusii Katika jamii ya Abagusii adhabu kwa maajuza watuhumiwa wa uchawi hutekelezwa kwa njia mbalimbali. Kama tulivyoshuhudia katika vyombo vya habari kumekuwapo na adhabu ya papo kwa hapo ya watuhumiwa wa uchawi. Hali hii ni tofauti na ilivyokuwa katika historia na utamaduni ambapo washukiwa walipitia aina fulani za majaribio yaliyolenga kuthibitisha tuhuma zozote dhidi yao kabla ya kuadhibiwa.Ni baada tu ya majaribio haya ndipo ambapo waliopatikana na hatia walipata adhabu yao. Isitoshe hali hii si ya kipekee katika jamii hii ya IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 12 kiafrika kwani tunaona hali kama hii ikitokea ulimwenguni ambapo mashtaka ya uhalifu wa uchawi yalifikia kiwango cha juu kutoka mwaka wa 1580 hadi 1630. Katika wakati wa kupambana na marekebisho ya vita vya dini ya Ulaya, wakati takriban watu elfu hamsini waliuawa, na baadhi ya maeneo yakichomwa ambapo takriban asilimia themanini ya waliochomwa walikuwa wanawake waliokuwa na umri zaidi ya miaka arobaini. Aidha kulikuwa na njia ainati Kihistoria za kwaadhibu washutumiwa wa uchawi auwale waliopatikana wakishiriki uchawi. Miongoni mwa adhabu hizo ni ile ya kifo, wengine kuchomwa,kunyongwa na hata kukatwa kichwa. Tukirejelea jamii ya Abagusii, tunapata kuwa miongoni mwa njiambalimbali zilizotumika katika kuwaadhibu wachawi ni kama ilivyoelezwa katika sehemu ifuatayo. i) Uingizaji wa Vifaa Vyenye Ncha Kali katika Sehemu za Siri za Watuhumiwa Mojawapo ya aina kali ya adhabu ya uchawi ni jaribu linalohusisha kuingiza vifaa vyenye ncha kali kwenye sehemu za siri za washukiwa.Mbali na ukali wake, aina hii ya adhabu inasemwa kuwa ya kufedhehesha sana.Utekelezaji wake unahusisha kuingizwa kwa kitu chenye ncha kali, hasa kijiti chenye umbo la mshale ndani ya sehemu za siri za mwathiriwa.Kifaa hiki kinaweza kuondolewa tu kwa njia ya upasuaji.Kutokana na namna ambayo adhabu hii inatekelezwa, wahasiriwa wa adhabu hii ni nadra sana kuishi . Washukiwa wa kiume pia wanaweza kuadhibiwa kwa njia hii pia pale ambapo vifaa vyenye ncha kali huingizwa kwenye sehemu zao za siri.Njia hii inafedhehesha zaidi wakati inahusisha kiungo cha uzazi cha mwanamke.Licha ya umuhimu wa kiungo hiki cha uzazi cha mwanamke katika kufanya mapenzi na kuendeleza ukoo na familia, kwa njia zingine uke hupewa mtazamo hasi. Miongoni mwa Abagusii ni mwiko kuitaja ile sehemu ya siri ya mwanamke (embere) hasa hadharani ikilinganishwa na ile ya mwanamume jambo ambalo linaweza kusemwa kuwa linajumuisha ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wanawake.Kwa hivyo,adhabu ya kuingiza kifaa chenye ncha kali katika uke wakati wa kuadhibiwa kwa mchawi inaonyesha jinsi wanaume wanavyowaona wake zao kama viumbe duni.Kama aina nyingine ya adhabu wanazozipokea wanawake kwa madai ya uchawi, adhabu hii inajumuisha ubaguzi wa jinsia dhidi ya wanawake. Kwa muda mrefu sasa, inaonekana kuwa adhabu ya uchawi katika jamii ya Abagusii inaonyesha kuwa kuna misukosuko katika mahusiano kati ya jinsia ya kike na ile ya kiume pale ambapo IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 13 jinsia ya kiume imependelewa sana.Kwa kweli, inaweza kusemwa kuwa, kuna mitazamo potovu kuhusu jinsia ya kike na hivyo basi majaribio ya uchawi ni njia tu ya kulazimisha mfumodume. Kulingana na wahojiwa wetu, jamii ya Abagusii huwachukulia wanawake kama watu ambao kila wakati wanasafiri (abaeti).Jambo hili linamaanisha kwamba,wawe katika nyumba za wazazi wao au katika ndoa, hawana makazi maalumu.Vilevile wanapoozwa na kwenda katika nyumba zao za ndoa,hubeba jina la wageni(abarwa isiko).Jina hili hutumiwa kuonyesha kuwa, mwanamke ni mpita njia tu na kama watu wengine ambao hawahusiani na jamii ile, wanawake hawa hawapewi haki sawa na wenzao wa kiume. Kwa jumla, wanawake wa Abagusii huchukuliwa kuwa viumbe dhaifu na hali hii ya kuwakumbushwa kila wakati kwamba wao si sawa na wanaume imewafanya kujidumaza.Kwa hivyo, dhuluma mbalimbali zinapofanywa dhidi yao, ni vigumu sana kuinua sauti zao kulalamika. i) Wachawi Kuchomwa Kuwepo kwa wachawi bado ni imani ya kijamii inayoendeshwa na wazo ambalo limechukuliwa kuwa la kawaida katika jamii za Kiafrika na jamii kadha nchini Kenya.Imani hizi za uchawi zimechochea adhabu kali ya wanaoshukiwa kuwa wachawi.Hivyo basi kuchomwa kwa kwa watu wanaoshukiwa kuwa wachawi katika jamii ya Abagusii ni jambo la kawida sana ambapo kesi hizi huripotiwa kwenye vyombo vya habari.Serikali imeweka juhudi nyingi hili kuzuia mauaji haya ya watuhumiwa wa uchawi ila haijafua dafu.Ingawa kitendo hiki cha kuwachoma watu kwa madai ya uchawi ni kitendo cha ukatili ambacho kinapaswa kuwa kimelaaniwa na jamii, hakuna suluhu yoyote imepatikana hadi sasa ili kukomesha kitendo hiki Wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya maajuza wanaoshukiwa kuwa wachawi katika kaunti ya Kisii limezua wasisiwasi katika eneo hili.Katika vyombo vya habari ni dhahiri kuwa maajuza huteketezwa kila kuchapo.Wauaji wao hudai kuwa maajuza hao hushiriki uchawi.Uchomaji wa wachawi hutumika kama njia ya kulipiza kisasi dhidi ya wanawake wazee jambo ambalo linaonekana kuleta vurugu. Kulingana na habari kutoka gazeti la taifa leo,mnamo Januari 14,wanawake wawili wazee walichomwa kiasi cha kutotambulika katika kijiji cha Omokonge,Kaunti ya Nyamira, kwa tuhuma za uchawi.Pauline Mogambi,95, na bintiye Rose Mogambi,53, waliuawa na wanakijiji IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 14 wenye hasira.Nyumba nane za watu wanaodaiwa kuwa wachawi pia zilichomwa moto.Baadhi ya watu ambao huchomwa wanaweza kuwa hawana hatia.Adhabu hii ni haramu kwani inamnyima mshukiwa haki ya kuishi. Ingawa wanaume na wanawake hujihusisha katika shughuli za uchawi, kesi zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari zinaonyesha asilimia kubwa ya waathiriwa ni wanawake.Mfumo wa jamii ya Abagusii kimsingi ni mfumodume.Wanaume tofauti na wanawake ni watu wanaoaminika kuwa wa kudumu katika jamii.Ingawa wanawake wanaweza kuonekana kuwa watu wa jamii au ukoo ule kwa sababu ya kuzaa watoto, mara nyingi wanachukuliwa kuwa watu wasio na uhusiano wa moja kwa moja na jamii ile kwa sababu hawana uhusiano wa damu na jamaa zao wa ndoa.Hivyo basi, wakati mwanamume ameshukiwa kufanya uchawi, ukoo unaweza kuzuiwa kumuua mwanamume yule kwa vikwazo vya uhusiano wa damu na hofu ya kumwaga damu ya jamaa yao. Kutokana na utafiti huu,shutuma za uchawi zinazosababisha uteketezaji wa maajuza wanaoshukiwa kuwa wachawi ni tabia ya kishenzi ambayo huidhinishwa na baadhi ya wanajamii ambapo vitendo hivi vimekithiri.Mauaji haya ambayo yamekuwa yakitokea Kisii kwa miongo mingi si mila au desturi za kitamaduni za watu wa Abagusii mbali ni vitendo vya ukatili uliokithiri vinavyochochewa na uchoyo, ubinafsi,chuki dhidi ya wanawake na dhana na maadili ya mfumo wa ubabedume ambao unashusha thamani maisha ya wanawake. ii) Wachawi Kufukuzwa Kutoka Koo Zao Adhabu hii uhusisha kutengwa kwa mtu au watu kutoka kwa kikundi fulani cha watu au jamii.Adhabu hii hutokea kutokana na ukweli kwamba mtu au watu wamekiuka sharia za kikundi Fulani au jamii hiyo.Kutoroshwa Katika jamii basi ni aina ya adhabu apatayo mtu aendeapo kinyume na matarajio ya jamii yao.Miongoni mwa Abagusii, washukiwa wa uchawi hulazimishwa kutoka Katika koo zao au hata jamii zao.Mara tu wanapofukuzwa kutoka koo zao, wao huwa kama wale watu waliougua ugonjwa wa ukoma katika Biblia kwa maana kwamba hakuna mwanajamii angetaka kuonekana akishirikiana nao. Watu hawa wanapotengwa na wanajamii inakuwa vigumu kushirikiana na wezao hivyo inawalazimu kuondoka kwa hiari yao wenyewe kwa sababu ya hisia za kukataliwa.Watu hawa huishia na kukaa katika vijiji au koo za kigeni ambapo shughuli zao hazijulikani.Jambo hili limetumika kama mojawapo ya sababu zinazoelezea ni kwa nini tunapata watu wengi kwa kijiji IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 15 kimoja ambao hawana nasaba zinazofanana.Watu hawa kwa kawaida huitwa ‘Abamenyi’.Iwapo badaye kuna ushahidi wa kutosha kwamba wamerekebisha tabia zao, wanaweza kuruhusiwa kurudi kwenye jamii yao. Hata hivyo, hali hii huweza kuwa tofauti pale ambapo mshukiwa anayefukuzwa hutokea kuwa mwanamke.Mwanamke aliyetengwa na jamii, mara nyingi harudi katika boma ya wazaziwe mbali huchagua kuoleka katika jamii nyingine.Imani za uchawi miongoni mwa Abagusii ni sababu mojawapo ilitumika kueleza kwa nini wanawake wa jamii ya Abagusii wameoleka katika jamii jirani kama vile wajaluo, wakipsigis na wamaasai. Ni muhimu kutambua kwamba Abagusii kama jamii nyingine za Kiafrika hutawaliwa na mfumo dume.Kwa hivyo, kumfukuza mwanamume kutoka jamii yake kuliaminika kuleta upungufu wa idadi ya watu katika ukoo huo haswa kama bado hao wanaume wana uwezo wa kuzalisha watoto.Kwa hivyo, jamii haingemwadhibu vikali mwanamume aliyeshukiwa kuwa mchawi kwani walipoomba msamaha waliweza kupewa faini nyepesi na kusamehewa kwa onyo la kutojihusisha tena na uovu huo. Mara kwa mara, wanaume wanaoshukiwa kuwa wachawi wanaweza kuwanyooshea kidole wake zao kwa lawama za kuwafundisha au kuwapa uchawi(kobaa rirogio) ambapo mwanamke huyo alilazimika kubeba hasira za wanajamii (Nyagaka Moraa).Kwa kweli, wanaume walipata msamaha ikiwa wangetangaza hadharani kwamba wake zao waliwaathiri kwa kuwafanyia uchawi. Katika tukio ambalo lilihusisha mwanamke kufukuzwa kutoka kwa nyumba yake kwa tuhuma za uchawi, hakuna hisia kali ya hasara inahisiwa ikilinganishwa na kumfukuza mwanamume ambaye anaonekana kama mzalishaji mali katika jamii.Mtazamo kwamba wanawake ni viumbe dhaifu na wanyenyekevu hufanya iwe rahisi kwao kufukuzwa. Katika jamii hii ya Abagusii, wanawake wanaoshutumiwa kwa uchawi hutoroshwa kutoka kwa familia zao na kupelekwa katika ‘kijiji cha wachawi’ambacho wakisii huita ‘Egetii kia Abarogi’.Wanawake pekee ndio hutoroshwa kwa sababu wao huonekana kama viumbe dhaifu ambao hawawezi kuzitetea haki zao.Ubaguzi unaopelekea kufukuzwa miongoni mwa Abagusii, ni ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wanawake.Hii kimsingi inatokana na dhana kwamba wanawake IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 16 huoleka kutoka ukoo mmoja kwenda mwingine na hivyo, ukoo utapoteza kidogo sana kwa kuwafukuza. Madhara Yanayotokana na Adhabu Wanazopokea Maajuza, Washutumiwa wa Uchawi Adhabu ya uchawi kwa maajuza wanaoshutumiwa yana athari mbaya si haba kwa mtuhumiwa na jamii kwa ujumla (Sambe 2017;Asamoah Gyadu 2015).Madhara haya yanaweza kuwa ya kijamii na kiuchumi na pia yanayoathiri maendeleo ya mtu binafsi kama ilivyofafanuliwa katika sehemu ifuatayo. i) Athari za Kijamii Zinazotokana na Adhabu ya Uchawi kwa Jnsia ya Kike Maajuza wanaotuhumiwa kuwa wachawi,haki zao za binadamu hukiukwa pakubwa.Kulingana na Igwe(2013) ukiukaji wa haki za binadamu ni silaha ya madaraka na utaratibu wa ukandamizaji wa wanawake walio katika nyadhifa dhaifu za kitamaduni katika jamii.Unyanyasaji humfanya aliyeshutumiwa kutengwa na wezake katika jamii anamoishi.Unyanyapaa hudumaza na kuzuia maendeleo ya kijamii na vilevile ya wanawake kwani wao hudharauliwa na watu wa familia zao. Katika maeneo na nyanja ambazo uchawi unaaminika kurithiwa, husababisha unyanyapaa zaidi kwa watoto wa mtuhumiwa.Watoto hawa hupokea dhihaka kutoka kwa wanajamii kuwa wao ni watoto wa mchawi na hata kuendeleza uchawi(Quarmyne 2011).Matokeo ya utafiti na pia mahojiano na wanawake ulidhibitisha madhara haya katika maisha ya walioshutumiwa pamoja na watoto wao. Mmoja wa wanawake aliyehojiwa alisema kuwa;’kifo cha ghafla cha mtoto wa pekee wa mwenzangu wa nyumbani kililaumiwa juu yangu’. Jambo ambalo lilisababisha unyanyapaa kwake na hata kwa watoto wake. Matokeo ya utafiti huu ilionyesha kwamba adhabu ya uchawi husababisha kifo.Kutokana na ukosefu wa taratibu sahihi na chanya za kuwaadhibu wanaoshtumiwa kuwa wachawi wananchi huchukua sheria mkononi jambo ambalo limesababisha kuuwawa kwa watuhumiwa kama inavyoripotiwa katika vyombo vya habari.Njia hii ya kuwaadhibu wachawi husababisha matatizo ya kisaikolojia kwa wanafamilia wanaoshuhudia kitendo hiki kikitendewa mmoja wao. Adhabu ya uchawi hufanya washutumiwa kukabiliwa na ukiukaji wa haki ambazo zinaanzia haki ya kuwa huru kutokana na unyanyasaji, haki ya kupata chakula, haki ya kuheshimu maoni ya IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 17 maajuza wanaotuhumiwa kuwa wachawi, haki ya malazi na kulindwa(Foxcroft na Secker,2010).Maajuza hawa hukabiliwa na kifungo na kulazimishwa kushiriki katika sherehe za kufukuza pepo walio ndani yao jambo ambalo linawaaharibu kisaikolojia.Kushindwa kwa serikali kutoa huduma mbadala za utunzaji kwa wale wanaotuhumiwa kwa shughuli za uchawi ni ukiukaji wa haki zao za kuhudumiwa au kulindwa Zaidi ya hayo, adhabu ya uchawi huwafanya watuhumiwa kutelekezwa na watoto wao wenyewe, familia na wanajamii.Jambo hili linawafanya kutopata huduma za kijamii(Monyenye 1997).Maajuza wengi walioshutumiwa kuwa wachawi wamekimbilia maeneo ya mjini ili kuepuka kutendewa mabaya zaidi.Jambo hili limewasababishia matatizo makubwa ya afya ya akili katika kujaribu kukabiliana na ulimwengu sambamba na usasa.(Di Domenico,1982). Vilevile, shutuma za uchawi husababisha kusambaratika kwa familia.Kwa vile watuhumiwa wengi wa uchawi ni wanawake,wengi wao uhama vitongoji vyao ili kuepuka adhabu kali na ata kifo.Katika hali hiyo, watuhumiwa hawa huweza kupoteza watoto wao na waume zao huweza kuwataliki ili kuepuka hofu ya kutambuliwa kama washiriki wa uchawi(Monyenye 1977).Hakika, kulingana na washiriki wetu, hii inaweza kueleza kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake waliotalikiwa na waume zao. Zaidi ya hayo, mahusiano baina ya majirani na wanajamii humomonyoka.Hii ni kwa sababu uchawi huonekana kuleta madhara kwa watu wengine katika jamii.Kama ilivyobainishwa na Asamoah Gyadu(2015) majirani na marafiki humshuku na kumtuhumu kila mmoja wakati wanaposhindwa kuiendeleza maisha yao jambo ambalo huvuruga maisha na uhusiano mwema kati ya marafiki na jamaa. ii) Athari za Kiuchumi Zinazotokana na Adhabu ya Uchawi Athari kadhaa za uchawi zinapatikana kutokana na adhabu ya uchawi kwa maajuza Katika jamii ya Abagusii.Ikizingatiwa kuwa wanawake wanaoadhibiwa kwa madai ya uchawi hunyanyapaliwa na kubaguliwa ambapo maendeleo yao ya kiuchumi na hadhi yao huathiriwa vibaya. Katika baadhi ya matukio, watuhumiwa wa uchawi hulazimika kuhama makazi yao na kuacha mali zao nyuma na hata katika hali mbaya vitu vyao huchomwa na kuharibiwa(Dovlo 2007).Katika matukio mengine, mali binafsi ya watuhumiwa hutwaliwa na washtaki wao na IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 18 jamaa wengine wanaounga mkono mashtaka hayo.Jambo hili hurudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi ya wanawake hawa na watoto wao na kuwafanya kuwa maskini maishani mwao.Ilibainishwa na mwanamke wakati wa mahojiano kuwa;’Baada ya kushtakiwa kwa kumuua mtoto wa jirani yangu, nilidharauliwa na wanajamii kisha nikapoteza njia yangu ya mapato na biashara ndogo ndogo ambayo nilikuwa nikifanya kwa sababu watu walikataa kuninunulia kwa vile waliniona mchawi, hii ilisababisha kuhama kwangu’.Kutokana na hili, inaweza kuonekana kuwa watuhumiwa wamewekwa katika hali ya kupoteza hadhi yao ya kiuchumi na njia zao za kujikimu kimaisha. Hitimisho Kwa ujumla, adhabu ya uchawi ina athari mbaya kwa ustawi miongoni mwa Abagusii.Kwa upande wa jinsia ni muhimu kutambua kuwa miongoni mwa Abagusii wanawake wanajumuisha asilimia kubwa ya uzalishaji mali.Kwa hivyo, kuwanyima kazi kupitia adhabu ya uchawi inapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo Kutokana na utafiti huu inaonekana kwamba, adhabu ya uchawi husababisha pengo la kiuchumi pale ambapo rasilimali na watu ambao wanaendeleza biashara hupotea.Inabainika kwamba washutumiwa pamoja na familia zao hutia kikomo katika shughuli zao za biashara jambo ambalo linadunisha maendeleo ya uchumi katika jamii. Aidha, kutokana na utafiti ilibainika kuwa,adhabu ya uchawi inarudisha nyuma na kuathiri vibaya tija ya kiuchumi.Hii ni kwa sababu katika mazingira mengi ya kifamilia na maisha ya kijamii, wanawake wazee huchukua jukumu la kuwalea wajukuu wao jambo ambalo linaruhusu kizazi kipya kujihusisha na shughuli za kiuchumi ambazo zinawezesha uzalishaji na mapato ya familia(Eboiyehi 2017).Hata hivyo, kwa tuhuma zilizopo maajuza wanalazimishwa kuondoka kwao nyumbani na pia katika jamii na kuacha pengo kubwa katika tija ya kijamii na kiuchumi.Hili lilithibitishwa na mwanamke mmoja katika mahojiano, ‘Nilipotuhumiwa kuwa mchawi na kaka wa marehemu mume wangu na baadhi ya wanafamilia yao, ilinibidi kuondoka nyumbani na kumuacha binti yangu mkubwa akimlea na kumtunza mtoto wake peke yake’. Utafiti pia umeonyesha kuwa miongoni mwa Abagusii, wanawake wana jukumu muhimu katika uzalishaji wa mali.Hakika wanawake ndio wanaojishughulisha zaidi kuliko wanaume kwa ajili IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 19 ya kujikimu kimaisha.Kwa hivyo, kuwanyima haki ya kujishughulisha za mambo ya kijamii kwa njia ya kuwaadhibu, kunainyang’anya jamii nguzo yake ya uzalishaji wa kiuchumi.Kwa hivyo miongoni mwa Abagusii, kuondolewa kwa wanawake katika jamii kwa madai ya uchawi husababisha hasara kubwa. Utafiti huu pia umeonyesha kwamba umiliki wa mali miongoni mwa Abagusii unahusishwa na wanaume mbali si wanawake.Kwa hivyo, ikiwa mwanamke atajihusisha na uzalishaji wa mali yoyote hawezi kudai umiliki.Hivyo, wanawake wanaozalisha mali kisha kudai umiliki wanadharauliwa na jamii.Wanaonekana kuwa sio wa kawaida kisha kuitwa wachawi.Hivyo basi,wanawake wengi wa Abagusii huondoka kwa hofu ya kuadhibiwa.Kimsingi, jambo hili linaua ile hamu ya kuzalisha mali miongoni mwa wanawake wa jamii ya Abagusii.Kwa upande wa jinsia inabainika kuwa wanawake ni wazalishaji mali na basi adhabu ya uchawi inapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla MAREJELEO Acton, H. B. ed., 1961. The philosophy of Punishment. London: Macmillan. Adegbola, A.A.E.ED.., 1983. Traditional Religion in West Africa. Ibadan: Daystar Press. Akama, S. et. at (2006).Ethnography of the Gusii of Western Kenya.The Edwin Millen Press.New York. Akawa and Kadayi (2006). Alan Macfarlane, witchcraft in Tudor and Stuart England, Psychology Press, 1999. Ashforth, Adam (2000). Madumo, A Man Bewitched. University of Chicago Press. Awolalu et.al. 1979. Yoruba Beliefs and Sacrificial Rites. London: Longman. Bahemuka, J (1982). Our Religious Heritage.Nairobi. Thomas Nelson and Sons Ltd. Bogonko, S (1977). Christian Missionary Education and its Impact on the Abagusii of Western Kenya 1909-1963 Nairobi Kenya Crawford, J. R. 1967. Witchcraft and Sorcery in Rhodesia.London: OxfordUniversity Press. Beauchamp, T. 1982. Philosophical Ethics: An introduction to Moral Philosophy. New York: Mc Craw-Hill Publishing Co. Behringer, W.2004. Witches and witch-Hunts.A Global History. Malden Massachusetts: Polity Press. IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 20 Bever, E (2002). “Witchcraft, Female Aggression and Power in the Early Modern Community’’. In Journal of Social History. Brooke, E. 1993. Women Healers through History. London: Women’s Press Ltd. Bryman, A. (2001).Social Research Methods.New York: Oxford University Press. Carlo, J.B. 1965. The World of witches.Glendinning: The University of Chicago Press. Crawford, J. R. 1967. Witchcraft and Sorcery in Rhodesia.London: OxfordUniversity Press. Cole, D.H. 1955. On the Origin of Equality. Chicago: the Great Books Foundations. Daniel A. Offiong. Witchcraft, Sorcery, Magic, Social order among the Ibibio of Nigeria. Evans-Prichard, E.E. 1937. Witchcraft, Oracles and Magic among the Azande. Oxford: Oxford Favret-Saada, Jeannne (December 1980). Deadly words: Witchraftin the Bocage. Cambridge University Press. Federici, S. (2004). Caliban and the Witch. Autonomedia. Federici, S. (2018). Witches, witch-hunting, and women. PM Press. Frankena, K.W. 1989. Ethics. New Delhi: Prentice Hall of India Private Ltd. Gaskil, M. 1998. “The Devil in the Shape of a Man: Witchcraft, Conflict and Belief in Jacobean England’’.In Historical Research. Gehman, J.R. 1989. African Traditional Religion in Biblical Perspective. Nairobi: Kesho Publications. Gibblin, J. 2002. “The Criminalization of Witchcraft and the Politics of Chieftainship: A history of Unyambuda in Uwanji, Southern Tanzania’’. In Crime in EastAfrica: Past and Present perspectives. Naivasha: The British Institute of Eastern Africa. HAYES s (1995). Christians Response to witchcraft and Society in Missionalia, vol.23(3 November. Holmes, R (1974) witchcraft in British History.London. Fredrick Miller Ltd. Hutton, Ronald (1999) The Triumph of the Moon: A History of Modern Pagan Witchcraft, Oxford, OUP. Julia, A. 1976. Plato’s Republic and Feminism. New York: Viking. Keeling, M. 1970. Morals in a Free Society. London: SCM Press Ltd. Kirby, J. (1994). „Cultural Change and Religious Conversion in West Africa‟, in T.D. Blakely et al, eds,.Religion in Africa.Experience and Expression,London, James Currey. IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 21 Kothari, R. C. (2004). Research Methodology: Methods and Techniques, New Delhi: New age International (P) Limited Publishers. Kothari, R. C (2008). Research Methodology: Methods and Techniques, New Delh: New age International Publishing Ltd. Levack, Brian P.ed.(2013) The Oxford Handbook of Witchcraft in Early Modern Europe and Colonial America. Mayer, U. P. (1954) Witches Grahamstown: Rhodes Univ.,Inaugural Lecture. Magesa, Laurenti, 1997; African Religion: the Moral Traditions of Abundant Life; Pauline publications Africa, Nairobi. Marwick, M.G. 1982. Witchcraft and Sorcery.Harmondsworth: Penguin Books. Murimi J.N (2010) Uchanganuzi wa Maoni Andishi ya Walimu wa Kiswahili kwenye insha za Wanafunzi katika Shule za Upili Wilayani Transzoia Magharibi.(Tasnifu ya Uzamili) Haijachapishwa. Ndeti K. (1972). The element of Akamba life.Nairobi East Africa Printing House Nthamburi, Z. (1991). From Mission to Church – A handbook of Christianity in East Africa.Uzima Press- Nairobi. Njogu, K. na Chimera, R. (1999). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation. Offiong, D.A. 1991. Witchcraft, Sorcery, Magic and Social Order among the Ibibio of Nigeria.Enugu, Nigeria: Dimension Publishing Co. Parrinder G. (1963) Witchcraft: European and African. London: Feber and Faber. Parrinder, G. 1963. Witchcraft: European and African. London: Faber and Faber. Ranger, T. (1978) „Protestant Missions in Africa: the Dialectic of Conversion in the AMEC in Eastern Zimbabwe, 1900-1950‟, in Religion in Africa. Ranger, T. (1980).„Introduction‟.Themes in the Christian History of Central Africa. Temples P. (1959) Borton Philosophy Paris: Presence African. Tinga, K.K., (1998). Cultural Practice of the Mijikenda at Cross roads: Divination, Healing Witchcraft and the Statutory Law. AAP. Thomson, J.J. 1994. “Goodness and Utilitarianism”. Proceedings and Addresses of the American Philosophical Association,67 (4):7-21 TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu: Oxford University Press. IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 22 TUKI, (2013), Kamusi ya Kiswahili Sanifu (toleo la 3) Nairobi: Oxford University Press. Wamitila, K. (2008). Kazi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi: Vide~Muwa Publishers. Wagner, G. 1970. The Bantu of Western Kenya. London: Oxford University Press. Walker, R. 1978 Kant: The Argument of Philosophers. London: Routledge and Kegan Paul. Wanyeki, L. Muthoni ed. (2003). Women and Land in Africa: Culture, Religion and Realizing Womenn’s Rights.London:Zed Books, 2003. Winker, G. and Degele, N. (2011). Intersectionality as Multi-Level Analysis: Dealing with Social Inequality, European Journal of Women’s Studies 18(1):51-66 Women International League for Peace and Freedom (2017). Outcome of CEDAW Review of Nigeria-More Action Needed to Implement the WPS Agebda WILPF. IJO- INTERNATIONAL JOURNAL OF SOCIAL SCIENCE AND HUMANITIES RESEARCH ( ISSN 2811-2466 ) Volume 06 | Issue 12 | December 2023 | http://ijojournals.com/index.php/ssh/index 23 ABSTRACT 1.0 Utangulizi Utekelezaji wa Adhabu kwa Wachawi Maajuza katika Jamii ya Abagusii i) Uingizaji wa Vifaa Vyenye Ncha Kali katika Sehemu za Siri za Watuhumiwa i) Wachawi Kuchomwa ii) Wachawi Kufukuzwa Kutoka Koo Zao i) Athari za Kijamii Zinazotokana na Adhabu ya Uchawi kwa Jnsia ya Kike ii) Athari za Kiuchumi Zinazotokana na Adhabu ya Uchawi MAREJELEO